Rais Magufuli akerwa Wanafunzi kukaa chini

0
145

Rais John Magufuli amewaagiza Viongozi wa wilaya ya Ubungo jijini Dar es salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha atakaporejea jijini humo, madarasa katika shule ya msingi King’ongo yawe yamekamilika na Wanafunzi hawakai chini.

Dkt Magufuli ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Kagera, mara baada ya kuzindua shule ya sekondari ya Wavulana ya Ihungo iliyopo mjini Bukoba iliyokarabatiwa na serikali ya Tanzania na Uingereza kutokana na kuharibiwa na tetemeko la ardhi lililoyokea septemba 10 mwaka 2016.

“Ninazungumza nikiwa Kagera, lakini nikienda Dar es salaam niyakute hayo madarasa yamekamilika na Wanafunzi hawakai chini,” ameagiza Rais Magufuli.

Ameeleza kuwa atakaporejea jijini Dar es salaam atakwenda kuitembelea shule hiyo kuona kama agizo lake limetekelezwa.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa haiwezekani kuwa amewapa watu madaraka, wanazunguka kwenye maeneo hayo lakini bado wanafunzi wanakaa chini.

“Hii ni dhambi kwangu kwamba nilikosea kuwachagua baadhi ya viongozi,” amesema Rais Magufuli.

Ukarabati wa shule hiyo ya sekondari ya Wavulana ya Ihungo umegharimu shilingi bilioni 10.9 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 6.1 zimetolewa na Serikali ya Uingereza.

Dkt Magufuli ametumia uzinduzi wa shule hiyo kumpongeza Balozi wa Uingereza nchini kwa ushirikiano ambao amekuwa akiutoa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.