Dkt. Michael: Vyama vya wafanyakazi chachu ya maendeleo

0
377

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt Francis Michael amesema vyama vya Wafanyakazi si wapiga kelele, bali vimekuwa chachu ya kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma na utendaji kazi Serikalini.

Akizungumza kwenye Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) jijini Dar es salaam Dkt Michael amesema dhana hiyo ni potofu na Watumishi hawatakiwi kuibeba, kwani shughuli za vyama hivyo ni sehemu nzuri ya kutatua changamoto mbalimbali za Watumishi na kujadili mipango itakayoboresha utendaji kwenye maeneo ya kazi.

Aidha, ametaka kusiwe na mvutano kati ya vyama vya Wafanyakazi na Menejimenti, bali kila jambo linaloibuliwa linatakiwa kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa maslahi ya pande zote.

Amewasihi Watumishi wa Umma, kupitia vyama vyao kuhakikisha wanaboresha mienendo na maadili yao ambayo yanajumuisha kutii Serikali kwa kutekeleza miongozo yake, kufahamu mipaka ya mamlaka zao, kufika kazini kwa wakati na kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Amesema mambo mengine yanayoonesha kama Watumishi wana maadili ni pamoja na kutunza mali za Umma na kutoa huduma bora.