Waliohusika na mauaji ya watu 17 wahukumiwa kunyongwa hadi kufa

0
154

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma imewahukumu kunyongwa hadi kufa Watuhumiwa 6 kati ya 9, baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya watu 17 wa familia moja yaliyotokea Februari 10 mwaka 2010 katika eneo la mgaranjabo lililoko kwenye manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Mahakama hiyo pia imewaachia huru Watuhumiwa wengine 3 wa kesi hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa hawana hatia katika makosa waliyoshtakiwa.

Washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Juma Mgaya, Aloyce Nyakumu, Nyakangara Biraso, Marwa Mgaya, Wambura na Sadock Ikaka ambao kwa pamoja wanadaiwa kushiriki mauaji hayo ambayo chanzo chake ni kulipiza kisasi. 

Akitoa hukumu hiyo hii leo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mustapher Siyani amesema kuwa, mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri juu ya watu hao kuhusika na tukio hilo la kinyama.

Amesema kutokana na ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa  mahakamani hapo, Watu hao sita walikuwa na nia ya dhati ya kuwaondolea uhai watu hao ambao miili yao ilikutwa na majeraha makubwa sehemu za kichwani, shingoni na mgongoni.