Madini yawapandisha kizimbani

0
405

Wafanyabiashara watatu raia wa kigeni na Mtanzania mmoja, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam kwa kosa la kukutwa na madini mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 42.

Wafanyabiashara hao Mohamed Hashim, Mohamed Mubarak Muwas, Mohamed Yoonus na Mehboob Rattansi wamefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon mbele Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa mahakama ya Kisutu, Godfrey Isaya.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kuongoza genge la uhalifu, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon amedai kuwa washtakiwa hao wametenda kosa hilo tarehe 8 mwezi huu jijini Dar es salaam kwa nia ya kujipatia faida kinyume na sheria.

Aidha katika kosa lingine ambalo ni la utakatishaji fedha, Wakili Wankyo amedai kuwa Washtakiwa wote wanadaiwa kujihusisha katika miamala ya fedha ya zaidi shilingi milioni arobaini na mbili wakati wakijua pesa hizo ni zao la kosa la kumiliki madini bila kuwa na kibali, hivyo kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha pesa kilichotajwa.

Baada ya kuwasomea washtakiwa mashitaka yao bila kutakiwa kujibu chochote, Wakili Wankyo amedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo kuomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.

Hata hivyo Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 03 ya mwaka 2021 imeahirishwa hadi tarehe 28 mwezi huu na washtakiwa wote wamerudishwa rumande.