Wawekezaji waliobadili matumizi ya ardhi kikaangoni

0
286


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ametoa muda wa  siku kumi kwa kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), kuwabaini na kuwanyang’anya maeneo Wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi za taifa ambao wamebadili matumizi ya ardhi kinyume na makubaliano ya mikataba yao.


 
Waziri Ndaki ametoa muda huo wakati alipotembelea Ranchi ya Usangu iliyopo wilayani Mbarali mkoani Mbeya, alipokuwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo na kufanya mkutano wa hadhara na baadhi ya Wawekezaji, Wakulima na Wafugaji ambao wanafanya shughuli zao katika ranchi hiyo.

Wakati wa mkutano huo imebainika kuwa, baadhi ya Wawekezaji waliopatiwa vitalu na NARCO kwa ajili ya kufuga na kulima malisho ya mifugo wamekuwa wakikodisha maeneo hayo kwa wakulima na wafugaji kinyume na mkataba.
 
“NARCO siku kumi nadhani zinawatosha kubaini watu wanaojiita Wawekezaji waliobadilisha matumizi ya ardhi ambayo siyo kufuga wala malisho wanyang’anywe maeneo kwa kuwa wameenda kinyume na utaratibu wa mkataba kati yao na NARCO, na mimi nitafuatilia nitapenda kupata taarifa mmepata wangapi na wangapi wamenyang’anywa kwa kuwa wameenda kinyume na utaratibu waliokubaliana,” amesema Waziri Ndaki.
 
Waziri Ndaki amelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya Wakulima na Wafugaji wa wilaya ya Mbarali kuwa wamekuwa wakikodishwa maeneo ya ranchi hiyo na Wawekezaji kwa shilingi elfu 20  kwa ekari moja kwa ajili ya kilimo na madebe kumi ya nafaka baada ya mavuno kwa kila ekari, huku wafugaji wakilipa takribanI shilingi milioni mbili kwa ekari moja katika kipindi cha miezi minne kwa ajili ya kulisha mifugo yao kwenye maeneo ya Wawekezaji ambao wamepatiwa vitalu na NARCO kwa mkataba wa kufuga au kulima malisho ya mifugo.


 
Amesisitiza kuwa mkataba wa NARCO na Wawekezaji kwa ajili ya kufugia mifugo na kulima malisho hauruhusu Wawekezaji kukodisha eneo kwa mtu mwingine kwa ajili ya shughuli zozote kwa kuwa maeneo ya ranchi za taifa ni mali ya NARCO.

Kuhusu deni la zaidi ya shilingi bilioni sita ambalo NARCO inawadai Wawekezaji waliopatiwa vitalu katika Ranchi za Taifa zilizopo kwenye maeneo mbalimbali nchini, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ameuagiza uongozi wa Kampuni hiyo kufikia tarehe 15 mwezi Februari mwaka  huu saa saba mchana awe amepata taarifa ya Wawekezaji waliolipa madeni yao pamoja na ambao bado hawajalipa kabla ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi.
 
“Wawekezaji wote ambao tunawadai hapa Usangu na kwenye ranchi zingine wote walipe pesa ya NARCO tulipokubaliana kwenye mkataba tulikubaliana mtalipa pesa, mlipe madeni yenu ifikapo tarehe 15 mwezi februari saa saba mchana muwe mmelipa madeni yenu,  tunataka NARCO ijiendeshe kibiashara, lakini sioni tukielekea kwenye kujiendesha kibiashara na moja ya matatizo yanayotufanya tusifike huko ni kulea watu wa namna hii,” amesisitiza Waziri Ndaki.
 
Ameagiza wale ambao hawatakuwa wamelipa hadi kufikia muda huo wanyang’anywe maeneo hayo ili wapatiwe watu wengine ambao wataweza kulipa kwa mujibu wa mkataba,  ili NARCO iweze kufikia malengo yake.
 
Kwa mujibu wa Waziri Ndaki, wizara  ya Mifugo na Uvuvi imefanya tathmini juu ya madeni hayo na kuagiza yalipwe katika viwango na tozo mpya zilizowekwa kwa sababu imejiridhisha kwamba kwa gharama hizo NARCO itaweza kujiendesha na kuhudumia vizuri ranchi zake.
 
 Amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Profesa Elisante Ole Gabriel kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuangalia namna ya kukodisha maeneo ya ranchi za taifa kwa wakulima ambao wanaweza kulima malisho ya mifugo ili kuondokana na migogoro ya wakulima kupata maeneo kwa ajili ya kilimo ili kujikwamua kiuchumi.
 
Kwa upande wake Profesa Ole Gabriel amesema atahakikisha anasimamia maelekeo yote yaliyotolewa na Waziri Ndaki likiwemo la Wawekezaji kulipa madeni ya vitalu walivyokodishwa ili NARCO inayomiliki maeneo hayo iweze kujiendesha kibiashara kama moja ya malengo ya kampuni hiyo kupitia maeneo yake.
 
Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amemaliza ziara yake ya  kikazi ya siku mbili mkoani Mbeya, ziara iliyokuwa na lengo la kufahamu changamoto zilizopo kwenye Ranchi ya Usangu ambayo ni moja ya ranchi zinazomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa.