Rais wa Msumbiji kufanya ziara nchini

0
271

Rais Felipe Nyusi wa Msumbiji anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini kuanzia kesho Januari 11.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Geita, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa, Rais Nyusi alipanga kufanya ziara nchini tangu mwaka 2020, lakini kutokana na ratiba ya Uchaguzi Mkuu hapa nchini, alisogeza mbele ziara hiyo.

“Ziara hii ya Rais Felipe Nyusi ni ziara ya kindugu ambayo ilipangwa kufanyika mwaka jana, lakini haikuweza kufanyika mapema mwaka jana kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na sababu mbalimbali hususan uchaguzi mkuu wa Tanzania,” amesema Profesa Kabudi.

Amesema dhumuni la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika maeneo anuai yakiwemo ya Kidiplomasia, Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii kama yalivyoasisiwa na vyama vya ukombozi vya nchi hizo.

“Mtakumbuka mahusiano haya ya nchi mbili yaliasisiwa na Viongozi waanzilishi wa nchi zetu huru yaani hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa upande wa Tanzani na Hayati Eduardo Mondlane aliyekuwa Mwasisi na Muanzilishi wa Frelimo na mahusiano hayo yameendelea hadi leo,” amesisitiza Profesa Kabudi.

Naye Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema, Rais huyo wa Msumbiji atawasili katika uwanja wa ndege wa Geitabmajira ya saa 4 asubuhi, hivyo amewaomba Wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kumpokea.

“Nawaomba wakazi wa Geita mjitokeze kwa wingi kumpokea mgeni wetu na pia ni wakati muafaka wa kutumia fursa hiyo kujiimarisha kiuchumi kupitia biashara tunazofanya, “amesema Mhandisi Gabriel.