Serikali yasisitiza usimamizi wa miradi inayotekeleza

0
157

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema miradi yote inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, lazima isimamiwe vizuri ili kuhakikisha inakuwa na viwango vinavyoendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo alipozungumza na Viongozi wa mkoa wa Ruvuma katika uwanja wa ndege wa Songea, akiwa njiani kuelekea jijini Dar es salaam.

Uwanja huo kwa sasa unakarabatiwa ili kuimarisha huduma za usafiri wa anga mkoani Ruvuma.

“Maelekezo ya Serikali kwenye maeneo yote muhimu ya miradi isimamiwe kwa kina na hasa thamani ya fedha na viwango vya ujenzi wa miradi yenyewe, tumeona Sekondari ya Tunduru, majengo ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga, barabara ya Mbinga-Mbamba Bay na uwanja wa ndege utaalamu umetumika na thamani ya fedha ipo,” amesema Waziri Mkuu.
 
Amefafanua kuwa, zaidi ya shilingi bilioni 37 zimetumika kuimarisha uwanja huo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma.

Ukarabati huo umehusisha njia ya kurukia ndege yenye uwezo wa kupokea abiria zaidi ya 150, jengo la abiria na maeneo ya maegesho yenye uwezo wa kuegesha ndege kubwa sita.

Uwanja huo wa ndege wa Songea utakapokamilika, utaruhusu ndege kutua usiku na mchana.