Bagamoyo na Mkuranga wamkuna Naibu Waziri Mabula

0
157

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amefurahishwa na hatua ya halmashauri za wilaya ya Mkuranga kununua vifaa vya upimaji na Bagamoyo kwa kuandaa mpango Kabambe wa matumizi bora ya Ardhi.

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi, viongozi wa mkoa wa pwani na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo mwishoni mwa wiki, wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi Dkt Mabula amesema uamuzi wa halmashauri kununua vifaa huku nyingine ikitenga fedha kwa ajili ya mpango kabambe ni kuonesha kuwa wakurugenzi wake wako makini kuhakikisha maeneo ya halmashauri hizo yanapangwa na kupimwa.

Akielezea uamuzi wa kununua vifaa vya upimaji katika halmashauri ya Mkuranga mkoa wa Pwani, Naibu Waziri Dkt Mabula alisema ni jukumu la halmashauri kuihudumia idara ya ardhi ili iweze kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi.

Amesema, halmashauri ikinunua vifaa kwa ajili ya idara ya ardhi itaiwezesha idara hiyo kupima maeneo mengi na hivyo kuifanya kuwa na maeneo mengi yaliyopimwa na kupangwa na kuepukana na migogoro ya ardhi.

Ameitaka halmashauri ya wilaya ya Mkuranga kuhakikisha kifaa ilichokabidhiwa kinatumiwa badala ya kukihifadhi na kushauri kuwa pale halmashauri nyingine katika mkoa huo zenye uhitaji wa kukitumia zitakapohitaji ziazimwe ili kuongeza kasi ya upimaji katika mkoa wa Pwani.

Kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo, Naibu Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliipongeza halmashauri hiyo kwa uamuzi wake wa kutenga fedha shilingi milioni 230 kwa ajili ya kuandaliwa mpango Kabambe wa mji wa Bagamoyo.