Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kusitishwa kwa mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Hamas wa Palestina katika ukanda wa Gaza.
Umoja huo umesema kuwa mapigano kati ya pande hizo mbili ni makali zaidi kuwahi kutokea katika eneo hilo tangu mwaka 2014.
Mapigano hayo kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Hamas yamezuka baada ya Wanamgambo hao kurusha makombora 370 ndani ya Israel na hivyo kuifanya nchi hiyo kulipiza kisasi kwa kufanya mashambulio ya anga.
Kwa sasa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika ukanda huo wa Gaza, – Nickolay Mladenov anashirikiana na Misri pamoja na pande zote zinazohusika katika mapigano hayo kwa lengo la kurejesha hali ya utulivu.
Hapo jana, ndege za Israel ziliyashambulia maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na kuharibu kituo cha televisheni kinachomilikiwa na wanamgambo wa Hamas na kuwaua raia watatu wa Palestina.
Habari zaidi kutoka eneo hilo zinasema kuwa kumekua na mapigano usiku wote wa kuamkia hii leo.