Mabehewa ya treni iliyopata ajali kuanza kuinuliwa asubuhi hii

0
176

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amesema kazi inayofuata baada ya kuwaondoa majeruhi wote wa ajali ya treni iliyotokea hapo jana, ni kuinua mabehewa sita yaliyoanguka.

Amesema kuwa kazi hiyo inaanza asubuhi hii kwa kushirikisha Wadau mbalimbali.

Dkt Mahenge amefafanua kuwa vifo kutokana na ajali hiyo iliyotokea jana saa moja kasorobo jioni katika eneo la Kigwa wilayani Bahi mkoani Dodoma ni vitatu, na si vinne kama alivyoeleza hapo awali.

Ametoa wito kwa Watanzania kupuuza taarifa zinazosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu idadi ya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo na kuwataka kuamini taarifa zinazotolewa na Mamlaka zinazohusika.

Amesisitiza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo ilipotokea ajali hiyo, ambapo tuta la reli limesombwa na maji.

Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma amesema tayari abiria wengine wote waliishaondolewa katika eneo la ajali na kupelekwa Bahi, na Shirika la Reli Tanzania (TRC) limefanya utaratibu wa kuwasafirisha kutoka Bahi kuelekea Manyoni – Singida ambapo watapata usafiri mwingine wa treni kwa ajili ya kuendelea na safari zao.

Treni hiyo ilikuwa inafanya safari zake za kawaida kutoka jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Kigoma.

Watu watatu wamefariki dunia na wengine zaidi ya sitini wamejeruhiwa katika ajali hiyo na wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya General na ile ya Bahi.