Ajali ya treni yaua watu watatu Dodoma

0
249

Watu watatu wamefariki dunia na wengine zaidi ya thelathini wamejeruhiwa, baada ya treni waliyokuwa wakisafiria kutoka jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Kigoma, kupata ajali katika eneo la Kigwa wilayani Bahi mkoani Dodoma.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameiambia TBC kuwa, ajali hiyo imetokea Jumamosi Januari 2 saa moja kasorobo jioni.

Amesema mabehewa sita ya treni hiyo yameanguka na kwamba chanzo cha ajali hiyo huenda ni mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo hilo.

Amesema majeruhi wa ajali hiyo wanapatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali zilizopo mkoani Dodoma.

Wakati treni hiyo inapata ajali, ilikuwa na abiria 720.