Mapambano dhidi ya ukatili kwa Wanawake na Watoto yasisitizwa

0
162

Watanzania wametakiwa kuwa Mabalozi ndani ya familia zao katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Kanisa la Mennonite Tanzania Dayosisi ya Mashariki Askofu Nelson Makori wakati wa kuhitimisha kongamano maalum la kuwajengea uelewa Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika kata ya Kitunda, juu ya vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ndani ya jamii.

Askofu Makori ,amesema vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto vinapaswa kupigwa vita na Watanzania wote.

“Maisha ya Wanawake na Watoto yana thamani kubwa sana kwa sababu Mungu amefanya miili yetu kama hekalu lake, hivyo unapomnyanyasa na kumdhalilisha mwanadamu mwenzako umemnyanyasa Mungu, unapomfanyia mwenzako mambo ya udhalimu umemfanyia Mungu,” amesema Askofu Makori.

Kwa Upande wake Diwani Mteule Kata ya Kitunda, – Victor Vedasto amesema uongozi wa kata hiyo utaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kulinda haki za Wanawake na Watoto.

“Naamini katika jamii ya Kitunda ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto umeshamiri, hivyo ni wakati wa kushirikiana pamoja kuhakikisha tunatokomeza kabisa tatizo hili na kama kuna hatua za kisheria zitahitajika kuchukuliwa dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo sitasita kutoa ushirikiano, “amesema Vedasto.

Nao baadhi ya Wanafunzi waliopewa mafunzo ya kukabiliana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wamesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuelimisha Jamii inayowazunguka kuachana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Awali kabla ya kuhitimishwa kwa kongamano hilo, Wanafunzi thelathini kutoka maeneo mbalimbali nchini wameshirki katika progarmu ya siku kumi na kufundishwa namna ya kukabiliana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ndani ya jamii na kukabidhiwa vyeti.