Mawasiliano ya barabara ya Makete kwenda Mbeya kupitia Ipelele yamekatika kwa muda sasa, kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani Makete mkoani Njombe.
Kufuatia hali hiyo, Maafisa kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Njombe wamefika katika eneo hilo na kuahidi kuwa kesho Mkandarasi atakuwa eneo la kazi kuanzia asubuhi ili kuhakikisha barabara hiyo inarejea katika hali ya kawaida na wasafiri na wasafirishaji wanaendelea na shughuli zao kwa ufanisi.
Maafisa hao wa TANROADS wamefika katika eneo hilo na kutoa ahadi hiyo baada ya Mbunge wa Makete, -Festo Sanga kufika eneo la mlima Ipelele majira ya asubuhi hii leo na kuwasiliana na Maafisa hao kuhusu hali ilivyo sasa katika eneo hilo.
Sanga alifika katika eneo hilo kwa lengo la kusaidiana na Wananchi kunasua moja ya magari ya abiria lililokuwa likielekea mkoani Mbeya baada ya kunasa katika eneo hilo la Ipelele.
Barabara ya Makete kwenda Mbeya ina umuhimu mkubwa kwa wakazi wa wilaya ya Makete, kwa kuwa imekuwa ikitumika zaidi kwa ajili ya usafirishaji wa mbao, viazi na matunda.
Wakazi wa wilaya ya Makete wameiomba Serikali kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami pamoja na barabara zingine zinazoiunganisha Makete mfano ile ya Chimala- Matamba – Kitulo na ile ya Kipengele Lupila.