Rais Magufuli azauia hoteli ya Sugu kubomolewa

0
795

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amemhakikishia aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joseph Mbilinyi maarufu kama ‘Sugu’ kuwa, hoteli yake ya Desderia inayodaiwa kujengwa kwenye chanzo cha maji haitabomolewa.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na uvumi kwamba hoteli hiyo itabomolewa kwa sababu ipo kwenye chanzo cha maji, lakini leo Chalamila ameeleza kuwa Rais Magufuli amemtuma aeleze kwamba mtu yeyote hatakiwi kubomoa hoteli hiyo.

“Kwa sababu huyu ni Mwekezaji kama Wawekezaji wengine na ikiwezekana kama tuna viwanja vingine upande huu wa Uzunguni basi moja ya watu wanaotakiwa kufaidika navyo ni pamoja na Sugu ambaye amekwishaanza kuwekeza hapa,” amesema Chalamila katika ujumbe huo alioagizwa na Rais Magufuli.

“Mmeona anatunza maji vizuri na maji yanatiririka vizuri na hayajakauka. Inawezekana kuna hoteli nyingine ambazo zimekausha maji sio hii, suala hili lisipelekee mvurugano wa kisiasa, mimi kauli yangu nasema maji ataendelea kuyatunza kama mnavyoona”, umesisitiza ujumbe huo wa Rais Magufuli.

Amehoji “Hoteli hii watu wa NEMC wanaijua, watu wa OSHA wanaijua, watu wa halmashauri wanaijua, mkuu wa mkoa anaijua, TRA wanaijua sasa kama wote tunaijua leo iweje tuseme iko kwenye maji, wakati inajengwa walikuwa wapi, wakati tunapima ardhi ilikuwa wapi au mto haukuwepo umekuja leo?.”

Kwa upande wake mmiliki wa hoteli hiyo ya Desderia, – Joseph Mbilinyi amesema kuwa anaamini ujumbe uliobebwa kwenye salamu za Rais Magufuli utasaidia kuleta hali ya kujiamini hata kwa Wafanyabiashara wengine, kama itatokea nafasi ya kuwekeza zaidi Mbeya.