TBC yamtembelea Mzee Bichuka, yajipanga kumsaidia kupata matibabu

0
407

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt Ayub Rioba Chacha na baadhi ya Watendaji wa shirika hilo, leo wamemtembelea Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini Hassan Bichuka nyumbani kwake Sinza jijini Dar es salaam.

Mzee Bichuka ambaye ameziimbia bendi mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja Msondo Ngoma na Sikinde, kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa macho.

Lengo la TBC kufika nyumbani kwa Mzee Bichuka ni kumjulia hali na pia kuzungumza naye namna ya kumsaidia kupata matibabu.

“TBC inatambua mchango wa wanamuziki wakongwe akiwemo Mzee Bichuka na ndio maana tumekuja kumtembelea ili kuangalia namna ya kumsaidia kupata msaada wa matibabu yake,” ameeleza Dkt Rioba.

Kwa upande wake Mzee Bichuka amesema kuwa amefurahishwa uamuzi wa uongozi wa TBC kwenda kumjulia hali na kwamba hatua hiyo inaonesha kuwa bado Wanamuziki wa zamani wanakumbukwa na shirika hilo.

“Mimi naumwa na naomba sana Watanzania wanisaidie kupata matibabu ya macho ambayo ndio yananisumbua sana” amesisitiza Mzee Bichuka

Pamoja na kusumbuliwa na macho, Mzee Bichuka anasumbuliwa na maradhi ya kisukari na shinikizo la damu na ameomba msaada wa kupatiwa matibabu ili arudi kwenye hali yake ya kawaida.