Wafanyakazi wa Mizani watakiwa kutochelewesha upimaji wa malori

0
153

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka watumishi wa mizani kutumia muda mfupi kupima na kuruhusu magari katika vituo vya mizani nchini ili kuondoa msongamano wa magari katika maeneo hayo.


Akizungumza mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja (OSIS) katika mizani ya Vigwaza mkoani Pwani, Mhandisi Kasekenya amesema Serikali imejipanga kuhakikisha hakutakuwa na ucheleweshaji wa malori katika vituo vya mizani hivyo kuwataka wasafirishaji kuzingatia sheria na kanuni wanapopakia mizigo ili kuepuka usumbufu.


“Lengo letu ni kuhakikisha magari yote yanabeba mizigo inayokubalika kisheria ili kuepuka faini na kulinda barabara tunazozijenga kwa fedha nyingi”, amesema Mhandisi Kasekenya.


Kasekenya ameelezea matokeo chanya yanayotarajiwa baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika ni kupungua kwa muda na gharama za usafirishaji, kuboresha usalama wa magari barabarani, kupunguza msongamano wa magari barabarani, kuondoa ukaguzi wa mara kwa mara kwa wasafirishaji hasa wa kuelekea mikoani na nchi jirani.


Aidha, amemtaka Mkandarasi China Railway Seventh Group anayejenga mradi huo kukamilisha kwa wakati na Serikali haitasikiliza visingizio vya mvua mara baada ya muda wa mkataba kumalizika.


Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Pwani, Mhandisi Yudas Msangi, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa mradi huo utasimamiwa kwa uangalifu na kwa kuzingatia viwango vilivyokubaliwa kimkataba na kutoa fursa za ajira kwa watanzania.


Msangi amefafanua kuwa zaidi ya magari 1700 yanapimwa kila siku katika mizani hiyo.


Zaidi ya shilingi bilioni 17 zinatumika katika utekelezaji wa mradi huo ulioanza tarehe 02/09/2020