Mawakili wapya 166 wa kujitegemea wakubaliwa na kupokelewa

0
188

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amewataka Mawakili wa kujitegemea kuwawakilisha vema wananchi katika kesi zao Mahakamani, kwa kufuata sheria na kanuni stahiki za uwakili.

Jaji Mkuu ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam mara baada ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili wapya 166 wa kujitegemea na kuongeza kuwa, baadhi ya Mawakili wamekuwa si waaminifu katika kazi zao.

“Mtakapowajibika vema katika kutekeleza majukumu yenu wateja wenu nao watafurahi, Ila kumbukeni kusimamia katiba na sheria za nchi , na kwa Mahakama mkiwa kama maafisa wa Mahakama,” amesema Jaji Mkuu wa Tanzania.

Ameongeza kuwa ni wajibu wa Mawakili hao kuhakikisha Wananchi hawaingizwi katika uvunjifu wa sheria na badala yake wazingatie sheria na nidhamu katika kazi hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt Evaristo Longopa amewataka Mawakili hao kuwa sehemu kubwa ya kuisaidia Mahakama katika kufikia maamuzi ya haki.

“Mtakuwa na wajibu kwa Mahakama na kuhakikisha mnaisaidia Mahakama kufikia kwenye maamuzi ya haki na yanayotolewa kwa wakati,” amesema Dkt Longopa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Dkt Rugemeleza Nshala amewataka Mawakili hao kujiweka sawa katika matumizi fasaha ya lugha za Kiswahili na Kiingereza ambazo ni nguzo muhimu katika kazi ya uwakili.