Rais Magufuli atunukiwa Tuzo ya uongozi

0
199

Uongozi wa Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly, umemtunuku Tuzo ya Uongozi Rais Dkt John Magufuli, baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wake, ambapo Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika na Dunia.
 
Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Magufuli wakati wa ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Philadelphia Gospel Assembly, Dkt Yohana Masinga, ibada iliyofanyika katika makao makuu ya kanisa hilo jijini Dodoma.
 
Baada ya kupokea tuzo hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na Rais mwenye hofu ya Mungu na katika hotuba na maelekezo yake kwa viongozi na watendaji wa Serikali amekuwa akisisitiza suala la kumtanguliza Mungu mbele katika kuwahudumia Wananchi.  
 
“Ama kwa hakika hofu ya Mungu aliyonayo kiongozi wetu ndiyo hasa siri ya kufanikiwa kwa uongozi wake na Taifa letu kwa ujumla, sote ni mashuhuda kwamba Tanzania chini ya uongozi wake imekuwa nchi ya mfano Afrika na Dunia kwa ujumla katika kupiga vita rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma, pamoja na kurejesha nidhamu ya kazi ambayo ilikuwa imepotea katika ofisi za umma,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.