Serikali imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho kupeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua.
Akitoa tamko la serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho mjini Dodoma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi kidogo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wanawasilisha barua zao.
Amesema baada ya siku hizo kupita serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua.