Serikali imewataka wakulima wa zao korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa wa korosho kutoka maeneo mbalimbali duniani, lengo likiwa ni kupata soko la uhakika la zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, ambapo Mbunge wa Mtwara Mjini, -Maftaha Nachuma alitaka kupata kauli ya serikali kuhusu bei ya korosho ambayo imeshuka katika msimu wa mwaka huu na kusababisha wakulima kugomea baadhi ya minada.
“Tunaendelea kuzungumza na wanunuzi wakubwa ili tujue ni nani atanunua korosho na kwa kiasi gani, hivyo tunawaomba wakulima waendelee kuwa watulivu, serikali inajitahidi kuhakikisha zao hilo linatafutiwa masoko, Korosho zitanunuliwa tu,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya ujenzi wa viwanda vya mbolea.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Neema Mgaya aliyetaka kujua serikali ina mpango gani katika kuwahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vya mbolea ili wakulima waweze kuipata kwa gharama nafuu.
Ameongeza kuwa viwanda vya mbolea vilivyopo nchini ni vichache na havitoshelezi mahitaji, hivyo kwa sasa kuna utaratibu wa kujenga viwanda vingine viwili, kimoja wilayani Kilwa mkoani Lindi na kingine kitajengwa mkoani Mtwara.
Kuhusu suala la wakulima wa mahindi kukosa soko, amesema kuwa ruhusa ya kuuza mahindi nje ya nchi ilishatolewa na jambo hilo lilikwishatolewa ufafanuzi na Wizara ya Kilimo.
Waziri Mkuu Majaliwa amefafanua kuwa licha ya kuwepo kwa ruhusa hiyo ya kuuza mahindi nje ya nchi, ni lazima serikali itambue kiasi gani kinachotolewa kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, hivyo muuzaji anatakiwa awasisilishe taarifa zake kwa wakuu wa wilaya.