Rais Xi Jinping ateta kwa simu na Rais Magufuli

0
185

Rais Xi Jinping wa China amempigia simu Rais John Magufuli ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo hasa katika masuala ya uchumi.

Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa muda wa saa moja, Rais Xi Jinping amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili na ameeleza kuwa kuchaguliwa kwake kumetokana na kazi nzuri iliyofanywa katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ambapo uchumi umeimarika zaidi na kwamba anaiona Tanzania kuwa nchi itakayoongoza kwa ukuaji wa uchumi Barani Afrika.

Rais huyo wa China pia amempongeza Rais Magufuli kwa namna Tanzania ilivyokabiliana na ugonjwa wa corona na ameeleza jinsi China inavyoendelea kukabiliana na ugonjwa huo.

Pongezi nyingine kwa Rais Magufuli ni kutokana na utekelezaji mzuri wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa na ujenzi wa bwawa la kuzalisha megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji na kuongeza kuwa China itaangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais Xi Jinping kwa kumpigia simu, kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuiongoza Tanzania kwa kipindi cha pili na kumpongeza kwa hatua za kimaendeleo zinazopigwa na Tanzania hasa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Rais Magufuli amemhakikishia Rais Xi Jinping kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na China uliodumu kwa takribani miaka 55 baada ya kuasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong na kwamba Tanzania itaendelea kuiunga mkono China katika masuala mbalimbali ya kimataifa.

Amesema Tanzania inawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka China kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji, utalii, ujenzi na biashara kwa manufaa pande zote mbili.

Aidha, Rais Magufuli ameiomba China kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji wa miradi mikubwa kwa kutoa mikopo nafuu na ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni wa kuzalisha megawati 358 za umeme katika mto Ruhudji, Megawati 222 za umeme katika mto Rumakali na ujenzi wa barabara Visiwani Zanzibar.