Vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini Nigeria vinaendelea kuwatafuta mamia ya Wanafunzi wa kiume ambao hawajulikani walipo mpaka sasa, baada ya watu wenye silaha kuwateka nyara katika shule ya sekondari ya Katsina iliyopo Kaskazini mwa Nigeria.
Kazi ya kuwatafuta Wanafunzi hao imekuwa ikifanyika usiku na mchana, na vyombo hivyo vya Ulinzi na Usalama vimekuwa vikishirikiana kuwatafuta Wanafunzi hao katika eneo lenye pori kubwa nje kidogo ya mji wa Kankara.
Kwa sasa, wazazi wa Wanafunzi hao wamekusanyika katika eneo la shule hiyo inayomilikiwa na Serikali kusubiri kupata taarifa kutoka kwa uongozi wa shule hiyo, kujua walipo watoto wao.
Watu hao wenye silaha hadi sasa hawajatoa dai lolote ili waweze kuwaachilia huru Wanafunzi hao.
Taarifa iliyotolewa awali na maafisa wa Serikali ya Nigeria ilieleza kuwa wanadhani ni Wanafunzi Kumi tu ndio wanaoendelea kushikiliwa na watu hao wenye silaha, kwa kuwa wengi wa waliotekwa nyara huenda walitoroka.