Waandishi wa habari kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jane John na Hamis Mwege wamepewa tuzo na chama cha mbio za Magari Duniani ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wa kuripoti habari zinazohusu mashindano ya mbio za magari.
Akizungumza baada ya kupewa tuzo hiyo, Jane John ambaye ni mwandishi nguli wa habari za michezo ametoa shukrani zake kwa chama hicho kwa kutambua mchango wake wa kuripoti habari na matukio yanayohusisha mbio za magari nchini.
“Najihisi furaha kutokana na tuzo hii niliyopatiwa, najiona nimezaliwa upya kwenye tasnia ya habari na nitaendelea kuripoti habari za michezo kwa weledi na ubunifu wa hali ya juu, nakishukuru chama hiki kwa kutambua mchango wangu hii inatoa fursa kwa waandishi wengine kujituma kwenye kazi zao” Amesem Jane John.
Naye mpiga picha Hamis Mwege, amesema mbio za magari ni miongoni mwa michezo anayoifuatilia sana hali inayomfanya kuchukua matukio ya picha kwa weledi na ustadi.
“Unajua mimi ni mpenzi wa mbio za magari kwa hiyo wakati nachukua picha za matukio haya hata sikuwaza kama kuna siku nitapewa tuzo, kwa kweli nakishukuru chama cha mbio za magari kwa kuthamini mchango wangu” Amesema Mwege.