Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania hasa vijana kutokubali kurubuniwa na baadhi ya watu wasio na mapenzi mema na Taifa, ambao wamekuwa wakitumia kundi hilo kuhatarisha amani ya nchi.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania na kuwasisitiza Watanzania wote kuwa na uzalendo na nchi yao.
Amesema uzalendo ni muhimu katika kujenga umoja wa kitaifa, na vijana ni zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wote hivyo wakipata misingi mizuri ya uzalendo kutakuwa na Taifa imara lenye nguvu na mshikamano.
“Uzalendo ndio utalifanya Taifa liendelee kujitegemea, hivyo ni muhimu suala hilo likapewa kipaumbele, msikubali kushawishiwa na Mtanzania yeyote anayetumiwa na watu wenye lengo la kutaka kuja kututawala, tusikubali lazima tuendelee kuwa huru na tulinde rasilimali kwa manufaa ya wote”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema vitendo vya uvunjifu wa amani na uharibifu wa miundombinu ni ukosefu wa uzalendo na kutothamini kodi zinazolipwa na wananchi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa, na kwamba vijana wakilelewa katika misingi ya uzalendo watakuwa walinzi bora wa rasilimali za Taifa.
Awali, Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, – Mwantumu Mahiza aliiomba Serikali iwapatie eneo jijini Dodoma kwa ajili ya kujenga kambi kuu ya kimataifa ambayo itakuwa na chuo cha ufundi, nyumba ya kulea vijana walioathirika na dawa za kulevya, kituo cha michezo, karakana, hoteli ya mafunzo, maeneo ya utalii na utamaduni, bustani za michezo na mashamba darasa.