Serikali imetoa waraka kuzuia watumishi wa umma waliohamishiwa Dodoma wakitokea Dar es salaam kurejea Dar es salaam mpaka watumishi hao waishi mkoani Dodoma kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt Laurean Ndumbaro na kuongeza kuwa, waraka huo umetolewa kufuatia ofisi hiyo kupokea barua zisizopungua mbili kila siku kutoka kwa watumishi waliohamishiwa Dodoma wakitokea Dar es salaam kuomba kurejea jijini Dar es salaam.
Dkt Ndumbaro ametaja baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikitolewa na watumishi wanaoomba kurejea jijini Dar es salaam kuwa ni kufuata matibabu.
Katibu Mkuu huyo wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma amewahakikishia wafanyakazi wote waliopo mkoani Dodoma kuwa, mkoa huo una hospitali ya Benjamini Mkapa inayoweza kutoa huduma zote kibingwa.