Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera imeanza kutoa mikopo ya vifaa badala ya fedha taslimu, kutokana na mikopo ya fedha kuwa na changamoto katika urejeshwaji, tatizo linalotokana na baadhi ya wanaokopeshwa kuzitumia fedha hizo kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mkopo wa pikipiki tatu zenye thamani ya shilingi milioni 7.8 kwa kikundi cha waendesha bodaboda cha Nidhamu Kazini, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Bukoba, Murshid Issa amesema kuwa, jumla ya shilingi milioni 166 zimekwishatolewa kama mikopo kwa mwaka huu wa fedha, kwa vikundi 17, kutokana na asilimia 10 ya makusanyo ya ndani.
“Kutoa fedha taslimu kuna vikwazo vingi, watu wakikopa hawalipi na hii inatokana na wengi wao kutumia fedha za mkopo kwa matumizi mengine, ndiyo maana tumeona kama mtu anataka kufuga mfano kuku tunampa vifaranga, au kama ni mwendesha bodaboda anapewa pikipiki,” amesema.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Limbe Moris amewataka vijana wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda, kutumia kipato wanachokipata kutokana na mikopo ya pikipiki, kuanzisha miradi mingine, ili kujiongezea kipato.
“Leo tumekabidhi pikipiki tatu, tuna mpango wa kutoa mkopo wa pikipiki 10 na kufikia Aprili mwaka kesho tutakuwa tumetoa pikipiki nyingine,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda katika manispaa hiyo, Abdulsalum Mashankara amesema kuwa wamejipanga kusimamia mikopo hiyo na kuhakikisha inarejeshwa kwa wakati.