Mfuko wa Bodi ya Barabara Tanzania umetishia kusitisha fedha za matengenezo ya barabara kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Manispaa ya Morogoro endapo ndani ya saa 24 itashindwa kufanya ukarabati wa barabara ya Kichangani iliyotelekezwa kwa zaidi ya miezi sita tangu miundombinu yake kuharibiwa na mvua.
Wakiwa katika ukaguzi wa barabara ndani ya Manispaa ya Morogoro, uongozi wa mfuko wa bodi ya barabara ukiongozwa na makamu mwenyekiti wa bodi hiyo umeeleza kutoridhishwa na hali ya barabara zilizopo katikati ya manispaa hiyo .
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TARURA Manispaa ya Morogoro, Mhandisi Mboka Nkwera amesema watahakikisha kasoro zote zilizobainishwa na bodi hiyo zinapatiwa ufumbuzi .
Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Benjamin Mziku amesema katika mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 7.5 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara mkoani Morogoro.
Licha ya serikali kutoa fedha za matengenezo ya barabara kila mwaka, bado kumekuwepo na changamoto ya usimamizi wa fedha hizo katika ukarabati wa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali hapa nchini.