TACAIDS: Wanawake wanaongoza kwa maambukizi ya UKIMWI

0
219

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani inayotarajiwa kufanyika Disemba Mosi mkoani Kilimanjaro.

Wakati siku hiyo ikiadhimishwa kwa lengo la kukuza uelewa juu ya ugonjwa huo na kuweka mikakati ya kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo hasa kwa vijana, kundi la vijana limetajwa kukumbwa zaidi na ugonjwa huo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016/2017.

Wakitoa maoni kuhusu kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa huo baadhi ya vijana jijini Dar es Salaam wamesema kuwa vijana wengi hufanya ngono zembe na hawapendi kupima kujua hali ya afya zao, hali inayopelekea kuendelea kuvisambaza kwa wengine.

Vincent Malima ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam anasema tatizo linalochangia maambukizi ni vijana wengine ni kupenda maisha ya urahisi, na vitu ghali bila kujituma na hivyo kuangukia mikononi mwa watu wasio wema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Richard Ngirwa amesema uwiano wa maambukizi ya UKIMWI yanaonesha kuwa wasichana/wanawake wana maambukizi makubwa zaidi kuliko wanaume.

Ngirwa amesema sababu ni kuwa wanawake ni wengi zaidi kuliko wanaume na pia sababu nyingine ni maumbile yao ambapo wao ni wapokeaji.

Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti Virusi vya UKIMWI ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wanafunzi kwenye shule na kuhimiza ngono salama.