Chaneli ya Utalii TBC mbioni kuzinduliwa

0
1991

Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Susan Mlawi ameelezea kuridhishwa na hatua iliyofikiwa ya uanzishwaji wa chaneli maalum ya Utalii ya shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mlawi ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati wa kikao maalum cha Makatibu wakuu wa sekta zinazohusika na masuala ya utalii na menejimenti ya TBC na kuongeza kuwa chaneli hiyo itazinduliwa mwezi Disemba mwaka huu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa hatua iliyofikiwa ya uanzishwaji wa chaneli hiyo maalum ya utalii ni kubwa na ya kuridhisha.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt Salehe Yusuf Mnemo ambaye amewaeleza washiriki wa kikao hicho kuwa suala la utalii ni la kitaifa na likipewa kipaumbe litakua na faida kubwa kwa Taifa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBC, – Dkt Ayub Rioba amesema kuwa chaneli hiyo itakayojulikana kama TANZANIA SAFARI itakuwa ni maalum kwa ajili ya kutangaza maliasili, utalii, vivutio na tamaduni zilizopo nchini .

Dkt Rioba ametoa wito kwa Watanzania wote hasa waandishi wa habari, kuandika na kutangaza mambo mazuri ya kimaendeleo ya Taifa ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya raia wa mataifa ya nje kuwa Bara la Afrika linatawaliwa na vita na njaa.

Mwezi Mei mwaka 2017 alipoitembelea TBC, Rais John Magufuli aliliagiza shirika hilo kuanzisha chaneli maalum itakayotangaza mambo mazuri na ya kuvutia yanayopatikana Tanzania, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kila mwaka.