Mkurugenzi wa manispaa ya Kigamboni mkoani Dar es salaam, -Ng’wilabuzu Ludigiji amesema kuwa kuna umuhimu kwa vituo vya afya nchini kutumia mashine za kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato.
Ludigiji amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti upotevu wa mapato na hivyo kuboresha utoaji wa huduma bora za afya kwa wagonjwa.
Mkurugenzi huyo wa manispaa ya Kigamboni ametoa kauli hiyo wakati akipokea msaada wa vitanda vya kulalia wagonjwa pamoja na vya kujifungulia vitakavyotumiwa na wagonjwa wanaolazwa katika kituo cha afya cha Kigamboni.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa NMB Kanda ya Dar es salaam, – Badru Iddi amesema kuwa benki hiyo ipo tayari kutoa mashine hizo za kielekroniki ili kuvisaidia vituo vya afya katika ukusanyaji mapato.
Tayari serikali imetoa shilingi milioni mia nne kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya akina mama katika kituo hicho cha afya cha Kigamboni, ujenzi ambao umefikia hatua ya kuezeka na itakapokamilika itasaidia akina mama wengi zaidi wanaofika katika kituo hicho kwa ajili ya kupatiwa matibabu.