Madini kuchangia 10% ya pato la Taifa hadi 2025

0
396

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewataka wataalamu wa jiolojia nchini kutekeleza wajibu wao kwa weledi ili kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa kutoka 5.2% mwaka 2019 hadi kufikia 10% mwaka 2025.

Mongella ametoa wito huo katika mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wanajiolojia nchini, unaofanyika jijini Mwanza na kushirikisha wataalamu pamoja na wadau wa jiolojia kutoka sekta mbalimbali zikiwemo za madini na nishati.

Rais wa Chama cha Wanajiolojia Tanzania, Prof. Abdulkarim Mruma, amesema ongezeko la mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa kutoka 3.2% mwaka 2012 hadi 5.2% mwaka jana, limetokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo mabadiliko ya sheria zinazosimamia maliasili na rasilimali za Taifa ya mwaka 2017.

Prof. Mruma amesema usimamizi makini utawezesha sekta ya madini kuchangia 10% ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, James Mataragio, amesema Serikali imejipanga kusambaza nishati ya gesi asilia ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya nishati hiyo ndani na nje ya nchi.

Kupitia mkutano huo utakaofikia tamati Novemba 29, baadhi ya wachimbaji wadogo watapata mafunzo kuhusu namna ya kuendesha uchimbaji wenye tija.