TFF: Karia hahusiki na fedha za CAF

0
298

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekanusha taarifa zinazomuhusisha rais wa shirikisho hilo Wallace Karia na malipo yanayodaiwa kusababisha kufungiwa kwa rais wa CAF Ahmad Ahmad kwa muda wa miaka mitano kwa matumizi mabaya ya fedha.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) kumfungia Ahmad ambaye anatuhumiwa kwa vitendo vya rushwa, ubadhirifu pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.

FIFA iliweka bayana kuwa, kiongozi huyo ambaye alikuwa ameshatangaza nia ya kugombea nafasi ya urais kwa mara ya pili huku nchi 46 kati ya zikimuunga mkono alikuwa amekiuka maadili ya kazi yake.

Katika taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo imesema, “itakumbukwa kuwa Mei 2017, Kamati ya Utendaji ya CAF ilipitisha uamuzi kuwa kila mwanachama wake ikiwemo TFF, kupatiwa mgawo wa dola za kimarekani laki moja ($ 100,000) ambazo ziligawanywa katika maeneo mbalimbali.”

Miongoni mwa fedha hizo ($ 100,000), dola 20,000 zilitakiwa kuwekwa kwenye akaunti binafsi ya Karia kwa ajili ya posho na majukumu mengine lakini, inaelezwa fedha hizo hazikuwekwa bali zote ziliingia kwenye akaunti ya TFF.

Baada ya mgao huo wa CAF kuingia kwenye akaunti ya TFF, jumla ya $ 80,000 zilielekezwa katika matumizi ya shughuli za maendeleo ya soka la vijana na Karia alielekeza fedha zilizobaki ($ 20,000) zitumike kwa shughuli mbalimbali za shirikisho kutokana na changamoto ya kifedha iliyokuwepo. Hivyo hakuna fedha ya CAF iliyowahi kuingizwa kwenye akaunti binafsi ya Karia.

Aidha, taarifa ya TFF imesema kuwa, Kamati ya Maadili ya FIFA iliyomfungia Rais Ahmad haikuzungumza chochote kuhusu fedha hizo kwenda kwa marais na wanachama wa CAF na kuanzia sasa haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote watakaoendelea kusambaza taarifa hizo za uongo.