Njia ya Marangu na upekee wake wa kupanda Mlima Kilimanjaro

0
349

Baada ya Njia ya Marangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro kushinda tuzo kutoka nchini China kwa kuwa njia bora zaidi ya kupanda kwenye mlima huo, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limefunga safari na kuikagua na kukuza uelewa kuhusu njia hiyo.

Wakiwa njiani, watumishi wa TBC wamejionea uzuri wa njia hiyo ambayo imepambwa na mandhari ya kuvutia, vivutio mbalimbali vidogo unavyoweza kutembelea kabla au baada ya kufika kileleni mwa Mlima Kilimanjaro.

Njia hiyo ambayo ni kongwe zaidi kati ya njia tano za kupanda mlima huo mrefu zaidi Afrika, ina huduma bora zaidi za malazi na mapumziko kuliko njia nyingine na pia inaelezwa kuwa ndiyo njia nyepesi zaidi kupanda.

Sifa nyingine ya njia hiyo ni kuwa ni njia pekee ambayo mtalii ataitumia kupanda na kuteremka. Mtalii anapopanda kupitia njia nyingine mfano Machame, Lemosho, Umbwe, Rongai hatorudi/hatoshuka kwa kutumia njia hizo hizo, bali atashuka kupitia njia ya Mweka.

Utofauti huo unampa faida mtalii anayetumia njia ya marangu kwani vitu ambavyo hakuviona wakati anapanda, anaweza kuviona wakati wa kiteremka.

Mlima Kilimanjaro ni wa kipekee duniani ambapo unapopanda utashuhudia kanda mbalimnali za hali ya hewa duniani.

Kutoka getini hadi kituo cha Mandara ni ukanda wa msitu wa mvua (rain forest), kutoka Mandara hadi Horombo ni ukanda wa msitu wa vichaka (heath moorland), kutoka Horombo hadi mita 5,000 (baada ya kituo cha Kibo) ni ukanda wa jangwa (alpine desert) na kutoka mita 5,000 hadi kileleni (mita 5,895) ni ukanda wa mawe na barafu (rock and ice).