Mlima Kilimanjaro na fursa za maisha kwa wananchi

0
283

Wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro wamesema kuwa Mlima wa Kilimanjaro kwao ni maisha, kwani umekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza na kuboresha maisha yao ya kila siku.

Wakizungumza na TBC kuhusu tuzo ambayo Njia ya Marangu ya kupanda kwenye mlima huo imepata, wamesema hiyo ni fahari kwao na inaonesha jitihada zao za kutunza mlima huo zimezaa matunda.

“Kupitia mlima [Kilimanjaro] nimeweza kusomesha watoto wangu, ninatunza familia,” amesema Aggrey Francis ambaye ni muongoza watalii.

Aidha, Victor Vicent maarufu Kiredio (jina alilopewa na wasaidia watalii wenzake) amesema fursa za utalii kupitia Mlima Kilimanjaro zimemsaidia kupata ufadhili wa masomo, na sasa yeye anasomesha watoto watano.

Wakieleza sababu za Njia ya Marangu kupata tuzo hiyo, wamesema njia hiyo ni bora na rahisi kupanda mlima, kuna huduma nzuri za vyoo na malazi na pia ushirikiano wa wadau katika kutunza mazingira.

Njia ya Marangu imeshinda tuzo hiyo iliyotolewa nchini China baada ya Kampuni ya Zara Tours kupelekea video inayoonesha upekee wa njia hiyo.

Mlima Kilimanjaro ni mlima mrefu zaidi Afrika na mlima mrefu zaidi duniani uliosimama wenyewe ukiwa na urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari.