Mkutano wa 13 wa Bunge waanza Dodoma

0
1802

Mkutano wa 13 wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaendelea jijini Dodoma.

Mkutano huo wa wiki mbili umeanza kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kuwaapisha wabunge wanne ambao watatu kati yao wanakula kiapo kwa mara ya pili ndani ya Bunge la 11.

Wabunge hao ni Mwita Waitara wa jimbo la Ukonga Jijini Dar es salaa, Julius Kalanga wa jimbo la Monduli mkoani Arusha na Zuberi Kuchauka wa jimbo la Liwale mkoani Lindi ambao ndio wamekula kiapo kwa mara ya pili na mwingine ni Thimotheo Mzava wa jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga.

Mbunge Waitara, Kalanga na Kuchauka wamechaguliwa katika majimbo yao baada ya kujiuzulu na kuhama kutoka vyama vyao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kushiriki katika uchaguzi mdogo wa ubunge, na Mzava amechukua nafasi hiyo baada ya kufariki dunia kwa Steven Ngonyani aliyekua akishikilia kiti hicho.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Bunge imesema kuwa jumla ya maswali 125 ya kawaida yataulizwa wakati wa mkutano huo wa 13 na maswali mengine 16 ya papo kwa papo yataulizwa kwa Waziri Mkuu.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Wabunge wengine wapya ambao tayari wamepita bila kupingwa na wengine watakaochaguliwa wataapishwa wakati wa mkutano wa 14 wa Bunge hilo unaotarajiwa kufanyika mwezi Januari mwaka 2019.