TAKUKURU yarejesha milioni 118 zilizokuwa zimechepushwa

0
712

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imefanikiwa kuokoa shilingi milioni 118.2 za mfadhili wa huduma za afya nchini ambazo zilikuwa zimechepushwa kwa njia ya udanganyifu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema fedha hizo mali ya shirika lisilo la kiserikali zilikamatwa kutoka kwa wahalifu mbalimbali nchini na ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kutokujiingiza kwenye vikundi vya kifedha ambavyo havijasajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Mara baada ya kukabidhiwa fedha hizo zilizokamatwa kutoka kwa wahalifu, mwakilishi wa taasisi inayojihusisha na masuala ya afya, Rehema Mkumbwa amesema fedha hizo zitatumika kutatua changamoto mbalimbali kwenye vituo vya afya hususani afya ya mama na mtoto huku akishukuru taasisi hiyo kwa namna ilivyojidhatiti kukabiliana na watu wanaohujumu fedha za umma na taasisi binafsi.

Katika hatua nyingine, Mbungo amesema kuwa TAKUKURU inafanya uchunguzi dhidi ya watumishi wanne waliokuwa waajiriwa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao wanashikiliwa kwa mahojiano kwa tuhuma za wizi pamoja na ubadhirifu wa shilingi milioni 541.3