Mfanyabiashara na bilionea maarufu nchini Zimbabwe, Ginimbi Genius Kadungure aliyefariki dunia kwenye ajali ya gari atazikwa katika jumba lake la kifahari.
Kadungure (36) alifariki pamoja na marafiki zake watatu baada ya gari yake aina ya Rolls-Royce Wraith kugongana na gari aina ya Honda Fit kisha kugonga mti na gari yake kuwaka moto.
Marehemu anazikwa leo nyumbani kwake katika nyumba maalum (mausoleum) kwa ajili ya kaburi lake.
Mwili wa bilionea huyo aliyekuwa akimiliki moja ya Night Club kubwa nchini humo, ulipelekwa kwenye nyumba hiyo ya starehe kabla ya kupelekwa nyumbani kwa shughuli za kuaga na mazishi.
Dada wa marehemu Juliet Kadungure amewaambia ‘The Herald’ kwamba kati ya vitu kaka yake alitaka vifanyike ni pamoja na asizikwe hadi marafiki zake waliopo nje ya nchi wafike pamoja na wageni wengine na kila mtu atakayehudhuria mazishi yake avae nguo nyeupe.
Aidha, baba wa marehemu amesema mwanae alitaka baada ya kuzikwa kwenye jumba hilo la kifahari, nyumba hiyo igeuzwe na kuwa hoteli.