Majaliwa ateuliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania

0
485

Waziri Mkuu Mstaafu, Majaliwa ameteuliwa tena na Rais Dkt. John Magufuli kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili.

Kabla ya kutangazwa kwa jina hilo bungeni, wabunge wote walikaa kimya kuashiria shauku ya kutaka kujua jina litakalotajwa ili walithibitishe.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alimwita mpambe wa Rais aliyetumwa kuleta jina hilo kutoka kwa Rais Magufuli.

Mpambe huyo alimkabidhi spika bahasha ambayo ilikuwa imegongwa mihuri sita ya siri na ndani yake kulikuwa na barua mbili ambapo moja Spika Ndugai aliisaini na kumrudishia mpambe wa Rais ambaye aliiweka kwenye begi lake na kisha kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

Baada ya kumtaja Majaliwa kuwa ndiye aliyeteuliwa, shangwe iliibuka bungeni huku wabunge wakielekea alikokuwa amekaa mteule huyo na kumsindikiza hadi kiti cha mbele ambako alielekezwa kuketi.

Baada ya tukio hilo kukamilika, Spika Ndugai amesitisha shughuli za bunge kwa muda ili wasifu wa mteule huyo uandaliwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kisha Bunge litathibitisha jina hilo kwa kulipigia kura.