Rais Dkt. Mwinyi amuapisha Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar

0
458

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amemuapisha Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya kiapo hicho,  Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ametoa pongezi kwa Rais Mwinyi kwa kumuamini na  kumteua kuwa msaidizi wake namba moja na kuahidi kwamba atamsaidia kwa asilimia mia moja.

Ameeleza kwamba uteuzi huo ameupokea vizuri nakufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na kuhakikisha malengo ya Serikali yaliyowekwa yanafikiwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema yeye akiwa Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali hatokuwa na muhali wa aina yoyote na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa kwa watu ambao hawatotimiza majukumu yao.

“ Wananchi wana mategemeo makubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hasa baada ya Rais wa Zanzibar kushinda uchaguzi mkuu kwa kishindo kikubwa.”

Malengo ndani ya Serikali ni kuhakikisha matumaini yanarejeshwa kama vile Rais alivyoahidi kuyatekeleza katika kampeni zake kipindi ambacho anaomba fursa ya kuchaguliwa kuwa Rais, amesema.

Hemed Suleiman Abdulla aliteuliwa jana na Rais Dk. Hussein Mwinyi ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba.