Timu za Al Ahly ya Misri na Esperance ya Tunisia zinacheza mchezo wa kwanza kati ya miwili ya fainali ya ligi ya mabingwa Barani Afrika katika mchezo unaofanyika jijini Alexandria nchini Misri.
Timu hizo zinakutana kwa mara ya tatu kwenye msimu huu baada ya kucheza mara mbili kwenye hatua ya makundi ambapo Al Ahly ilishinda bao moja kwa sifuri nchini Tunisia na kutoka suluhu kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa nchini Misri.
Mjumbe wa bodi ya Al Ahly, – Khaled Mortagy amesema kuwa wanatarajia michezo hiyo miwili ya fainali itakuwa migumu kutokana na matokeo ya hatua ya makundi zilipokutana timu hizo ambapo amewataka wachezaji wa kikosi hicho kusahau matokeo ya michezo iliyopita na kupambana ili kutwaa taji hilo.
Jambo zuri kwa Al Ahly ni kurejea kwa mfungaji wao bora Walid Azaro, – raia wa Morocco aliyekuwa anauguza majeraha aliyoyapata kwenye mchezo dhidi ya Entente Setif ya Algeria kwenye mchezo wa nusu fainali.
Mabingwa wa kihistoria Al Ahly wenye makombe nane ya ligi ya mabingwa Barani Afrika, wanaingia kulisaka taji la tisa kwenye michuano hiyo huku Esperance wakiliwinda taji la tatu.