Kila mmoja ana wajibu wa kulinda amani

0
352

Wananchi wamehimizwa kulinda amani na utulivu wakati huu wa uchaguzi mkuu wa kuwapata viongozi wa kitaifa.

Rai hiyo imetolewa wakati wa kongamano la amani la viongozi wa dini lenye kaulimbiu isemayo “Amani Yetu, Maendeleo Yetu.”

Akiwakilisha Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Flornce Rwehumbiza amesema utaratibu wa kulinda amani na kuwapa watu haki zao ni wajibu wa kila mtu.

“Sisi kama viongozi wa dini ni kazi yetu ni kupiga baragamu wakati huu wa uchaguzi na amani hiyo italindwa kila mtu akitimiza wajibu wake kulinda amani,” amesema mwakilishi wa TEC, Fr. Florence Rwehumbiza.

Naye Imamu wa Msikiti wa Mtoro jijini Dar es Salaam, Othaman Khamisi amesema mani na utulivu vikitawala katika nchi watu wake wataweza kuabudu kwa uhuru na utulivu popote walipo.

“Wanaomba kuchaguliwa kuwa viongozi na wanaokwenda kuchagua viongozi wana wajibu wa kulinda amani ya nchi,” amesema Imamu Khamisi.

Kwa upande wake Askofu Zachariah Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Tanzania amesema kila kiongozi anapaswa kuchunga ndimi yake wakati na baada ya uchaguzi ili kuepusha moto ma machafuko katika taifa.

“Kuchunga ndimi zetu ndiyo silaha ya kuepuka machafuko kwani sisi sote ni wadau wa amani hivyo ni vyema kila mtu anapaswa kulinda amani hiyo.”

Pia amelipongeza Jeshi la Polisi kwakuendelea kuimarisha amani na utulivu wa nchi wakati huu wa uchaguzi.

“Kila mmoja wetu akitoa ushirikiano unaostahili kwa Jeshi la Polisi wakati huu wa uchaguzi naamini kila jambo litakwenda vizuri,” amehitimisha Kakobe.