Watanzania wahimizwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo

0
240

Watanzania wamehimizwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa kushiriki katika michezo mbalimbali, itakayowezesha Taifa kusonga mbele.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Wilaya Temeke, Lusubilo Mwaka katika bonanza maalum la kumuenzi Baba wa Taifa lililofanyika katika kiwanja kipya cha mpira wa miguu Makangarawe kilichopo Manisapaa Temeke jijini Dar es Salaam.

“Ili kulijenga Taifa ambalo watu wake wana afya njema na imara ni muhimu jamii ya kitanzania kutambua nafasi ya michezo katika kujenga afya ya mwili,” amesema Lusubilo.

Aidha Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuhakikisha miundombinu mbalimbali ikiwemo viwanja vya michezo vinaboreshwa, ili kuibua vipaji vipya vitakavyoitangaza nchi na kutoa fursa ya ajira kwa vijana na jamii nzima kwa ujumla.

Baadhi ya wadau wa michezo walioshiriki bonanza hilo la kumuenzi ambalo huadhimishwa Oktoba 14 kila mwaka, wamesema Manisapaa ya Temeke ni ya kuiga katika suala zima la michezo huku wakishauri vijana na watu wa rika zote kupenda michezo kwa maendeleo ya Taifa.