Waliodanganya umri Benin watupwa jela

0
1869

Wachezaji kumi wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 nchini Benin na Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini humo Anjorin Moucharafou wamehukumiwa kifungo jela kwa kosa la kudanganya umri.

Mahakama ya mji wa Cotonou imewakuta na hatia wachezaji hao baada ya vipimo vya MRI kubaini umri wao sahihi.

Mwezi Septemba mwaka huu,  wachezaji hao  kumi wa timu ya vijana  ya Benin walikwenda nchini Niger kushiriki michuano ya awali ya kufuzu kwa michuano ya Afrika ya vijana na walipopimwa walikutwa wamezidi umri na hivyo nchi hiyo kuondoshwa kwenye michuano hiyo.

Wachezaji hao kumi watatumikia kifungo cha miezi sita jela na kuzuiliwa kucheza soka kwa kipindi cha miezi mitano.

Kwa upande wake Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini Benin, – Anjorin Moucharafou  atatumikia kifungo cha miezi 12 jela na amefungiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa kipindi cha miezi kumi.