Bodi ya Filamu Tanzania yakanusha kutoa tozo mpya

0
424

Kufuatia kusambaa kwa taarifa kwenye mitandao kuwa Bodi ya Filamu Tanzania imetoa tozo mpya kwa waandaaji wa maudhui, bodi hiyo imeeleza kusikitishwa na usambaaji wa taarifa hizo ilizosema kwamba ni za uongo.

Mamlaka hiyo imesema kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote na kwamba zinalenga kuzua taharuki na kuupotosha umma kuhusu utoaji wa huduma za bodi na hivyo bodi haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakaye husika na usambazaji wa taarifa hizo.

Bodi hiyo imeueleza umma kwamba Kanuni za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ambazo zilichapishwa kwa tangazo Na. 488 lililotolewa kwenye gazeti la serikali toleo Na. 26 la mwezi Juni 2020 zilitokana na maoni ya wadau ambayo yalipelekea kushushwa kwa tozo zilizokuwa katika kanuni za mwaka 2011 tofauti na taarifa inayosambazwa.

Bodi ya Filamu imesema kuwa inaendelea kuboresha kanuni hizo kwa kuweka mazingira rafiki kadri inavyopokea maoni ya wadai wa filamu.