Serikali kuendelea kuboresha sekta ya afya

0
1812

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

Amesema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma muhimu hasa zile za maabara, upasuaji na mama na mtoto.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Malindi wilayani Lushoto baada ya kutembelea jengo la soko la mboga la Malindi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Tanga.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa serikali imejipanga vizuri katika kuboresha sekta ya afya ndio maana imeongeza bajeti ya kununulia dawa kutoka shilingi bilioni 31 kwa mwaka hadi kufikia shilingi bilioni 269.

“Hatutaki tena kusikia mgonjwa anaenda hospitali na kukosa dawa biashara hiyo tumeimaliza, Rais Dkt. John Magufuli ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa”, amefafanua Waziri Mkuu.

Amesema kuwa katika wilaya ya Lushoto, serikali imetenga shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya vituo vya afya vya kata za Kangagai, Mnazi na Mlola.

“Halmashauri wekeni mpango thabiti wa kujenga wodi mbili kati yake moja ya wanaume na nyingine ya wanawake, lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia mradi huo wa ujenzi wa soko hilo la mboga la Malindi, Waziri Mkuu amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya huduma zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii nchini.

Waziri Mkuu ametaja huduma nyingine zinazotolewa na serikali kwa wananchi kuwa ni pamoja na afya, elimu na maji.

Hivyo, amewataka wakazi wa kata hiyo ya Malindi kutumia vizuri soko hilo ambalo linatoa fursa kwao kufanya biashara katika eneo zuri na kuwawezesha kuuza bidhaa zao zikiwa katika ubora.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, -Ikupa Mwasyoge amesema kuwa kukamilika kwa soko hilo kutainufaisha halmashauri na wananchi.

Ikupa amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo la soko la ghorofa mbili lililojengwa kwa awamu mbili ulianza mwaka 2011 na umekamilika mwezi Septemba mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 1.1.