Dkt. Magufuli: Tutamaliza kero ya mafuriko jijini Dar es Salaam

0
559

Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Magufuli ameahidi kumaliza kero ya mafuriko jijini Dar es Salaam endapo akichaguliwa kuongoza kwa muhula wa pili.

Dkt. Magufuli ametoa ahadi hiyo wakati akizingumza na maelfu ya wakazi wa jijini hilo waliojitokeza katika Uwanja wa Tanganyika Packers wakati akihitimisha kampeni zake kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema kwa kushirikiana na wabunge na madiwani wa CCM ambapo watachaguliwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu, atahakikisha wanaboresha miundombinu ili mvua zinaponyesha, kusiwe na mafuriko.

“… Dar es Salaam tumepanga kuondoa hii kero mvua zinaponyesha maji yanajaa. Mtu una unga wako wa ugali, unasombwa na maji. Tunataka tushughulikie suala lote la mafuriko yanayotokea Dar es Salaam,” Dkt. @Magufuli

Mbali na hilo ameahidi kuboresha huduma za afya, ujenzi wa viwanda, ajira kwa vijana, na ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha usafiri ma usafirishaji kwani Dar es Salaam ni kitovu cha uchumi wa Tanzania.

Dkt. Magufuli amehitimisha kampeni zake kwa mkoa wa Dar es Salaam. Hata hivyo amewaomba radhi wakazi wa baadhi ya mikoa ambayo hatoweza kufika kwani licha ya kuwa kwenye kampeni, bado anatakiwa kuiendesha serikali.

Amewaomba wananchi wa mikoa hiyo kama Ruvuma, Katavi, mikoa ya Pemba na maeneo mengine kuwasikiliza wale aliowatuma huko akiwepo mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikweti.