Marekani imetangaza mpango wake wa kuwatuma zaidi ya askari elfu tano kwenda kusaidia kulinda maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Mexico, baada ya maelfu ya wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kati kujiunga na msafara wa wahamiaji wanaotaka kuingia nchini Marekani.
Mpango huo umetangazwa na Rais Donald Trump, huku baadhi ya wachambuzi wa masuasa ya kiuchumi wakisema kuwa idadi hiyo ya askari wanaotumwa kulinda maeneo hayo ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Habari zaidi kutoka nchini Marekani zinasema kuwa tayari askari mia nane wameishaelekea katika jimbo la Texas ambalo nalo ni eneo la mpaka wa nchi hiyo na mexico na wengine katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na majimbo ya California na Arizona.
Wakati marekani ikitangaza mpango huo, mamia ya wahamiaji kutoka Honduras wamevuka mto kuingia nchini Mexico, likiwa ni kundi jipya la wahamiaji wanaoelekea nchini Marekani.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya wahamiaji elfu saba wako njiani kuelekea nchini Marekani hivi sasa.
Maafisa wa uhamiaji nchini Marekani wamesema kuwa katika kipindi cha wiki tatu zilizopita,takribani wahamiaji elfu moja na mia tisa wamekua wakivuka mpaka kinyume cha sheria kila siku na kuingia nchini humo.