Mahrez amlilia Vishai

0
2006

Winga wa Manchester City, – Riyad Mahrez amesema kuwa mmiliki wa klabu ya Leicester City  marehemu Vishai  Rivahanapraha  alikuwa kama baba kwake na ilimuwia vigumu kupata usingizi kabla ya mchezo wa hivi karibuni dhidi ya Tottenham.

Mahrez amesema kuwa goli pekee na la ushindi aliloifungia  City dhidi ya Spurs ni kwa ajili ya marehemu Vishai na kwamba Bilionea huyo alikuwa mtu wa kipekee kwake na katika kipindi cha miaka minne na nusu alichokuwa Leicester wamefanya mambo mengi ambayo yanabaki kuwa kumbukumbu isiyofutika katika kichwa chake.

Nyota huyo wa kimataifa wa Algeria aliitumikia Leicester katika michezo 179 kati ya mwaka 2014 hadi 2018 na kuwasaidia kutwaa taji la ligi kuu ya England mwaka 2016 ambapo pia alitangazwa kuwa mchezaji bora.

Kwa mujibu wa Mahrez, habari za kifo cha Vishai na wenzake zimemuumiza sana na anaungana na klabu hiyo pamoja na wote walioguswa katika kipindi hiki cha majonzi.

Mahrez aliifungia City bao pekee na la ushindi katika dakika ya sita  katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Wembley,  ushindi unaowafanya City kukwea kileleni kwenye msimamo wa ligi ya England wakiwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga ambapo wamefikisha alama 26 sawa na Liverpool.

Katika hatua nyingine,  salamu za rambirambi zimeendelea kutolewa na watu mbalimbali mashuhuri kufuatia kifo cha  mmiliki huyo wa klabu ya Leicester City  kilichotokana na ajali ya helikopta Jumamosi iliyopita nje ya uwanja wa timu hiyo wa King Power.

Helikopta hiyo ambayo ni binafsi ilianguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka kwenye uwanja huo ambapo mmiliki huyo wa timu ya Leicester City FC alikuwa akirejea nyumbani mara baada ya kutazama mchezo baina ya timu yake na West Ham United.