Polepole: Wapinzani kushirikiana hakuzuii ushindi

0
426

Chama cha Mapinduzi kimesema kuwa kinasubiria kwa hamu ushirikiano wa baadhi ya vyama vya upinzani, kwani kushirikiana kwao hakutazuia CCM kuibuka washindi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020.

Akitoa tathmini ya mwenendo wa kampeni za chama hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama hicho kimeendelea na kampeni za kistaarabu na kitapata ushindi wa kishindo mwaka huu.

Kauli yake imekuja siku chache baada ya CHADEMA na ACT Wazalendo kuonesha nia ya kutaka kushirikiana katika ngazi ya Urais, jambo ambalo limepokelewa kwa mitazamo tofauti na wananchi.

Mbali na hilo amewataka Watanzania kupuunza baadhi ya hoja ambazo amesema si za ukweli zinazoenezwa na wagombea wa upinzani ikiwemo madai kuwa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) haikaguliwa matumizi yake, ununuzi wa ndege uliliwa nje ya bajeti na kwamba viwanja vya ndege vinajengwa kwa kuangalia maeneo walimotoka viongozi.

Akitolea mfano Uwanja wa Ndege wa Mpanda, Polepole amesema “… haukujengwa kwa sababu ya Mizengo Kayanza Peter Pinda. Wengi wanaotumia uwanja huo ni watalii wanaokwenda Mbuga ya Wanyama ya Katavi.”

Ameongeza kuwa, kwa tathmini ya CCM, endapo Watanzania wangepiga kura Jumatano (Septemba 23, 2020), mgombea Urais wa chama hicho, Dkt. Magufuli angepata kura asilimia 89.5 ya kura zote halali.

Kuhusu madai kuwa Dkt. Magufuli anatumia mamlaka ya Urais kwenye kampeni, Polepole amesema kuwa licha ya kuwa kampeni zinaendelea lakini serikali bado ipo kazini na kwamba Rais anakoma kushika wadhifa huo pale mwingine anapoapishwa.