Membe: Nimepima afya yangu Dubai, nipo imara kuendelea na kampeni

0
187

Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Bernard Membe amerejea nchini Septemba 15, 2020 akitokea Dubai baada ya kumaliza shughuli zake huko na kwamba yupo imara kuendelea na kampeni za uchaguzi mkuu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Membe amekanusha tetesi zilizokuwa zimeenezwa kuwa ni mgonjwa na hajulikani alipokuwa.

Membe amesema alikuwa Dubai kwa sababu za kibiashara kwani yeye ni mjumbe wa bodi ya kampuni kubwa mjini humo na hakuweza kuhudhuria vikao viwili mfululizo kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Aidha, ameongeza kuwa, akiwa Dubai alitumia fursa hiyo kufanya uchunguzi wa kiafya na yeye ni mzima wa afya na yupo tayari kuendelea na kampeni.

Mwanadiplomasia huyo amesema ana uzoefu na chaguzi za urais kwani ameshiriki chaguzi sita nchini na chaguzi 12 Afrika.

“Lazima kwanza ujipange, pili, lazima muwe na fedha, tatu, lazima muwe na timu ya uchaguzi (timu ya ushindi), nne, lazima muwe na ilani ya kuinadi na tano uwe na wabunge na madiwani wa kuwanadi na kuwashika mkono kote nchini.”

Membe aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kuanzia mwaka 2007 hadi 2015.